PATA HABARI ZA KILIMO BONYEZA HAPA

PATA HABARI ZA KILIMO BONYEZA HAPA
MKULIMA JEMBE PERUZI HAPA

MICHEZO

MICHEZO

TUPO KWA KISHINDO POPOTE.

PERUZI HABARI HAPA.

Monday, September 3, 2018

Lugola Akerwa na Mgambo Kuwapiga Kikatili Wananchi.....Atoa Onyo Kwa Walimu Wanaotumia Nguvu Nyingi Kuwapiga Wanafunzi

Na Felix Mwagara, MOHA
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amelaani tukio lililofanywa na Mgambo wa Jiji la Dar es salaam akisema ni la kihuni, kishenzi na kinyama na halipaswi kufumbiwa macho na wapenda amani, watetezi wa haki za binadamu na wananchi wote kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa Kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza, Lugola alisema Serikali inalaani vikali tukio hilo ambalo lililotokea wiki iliyopita jijini humo, na kutokana na unyama huo tayari hatua za kisheria zimeanza kuchukuliwa.

“Jeshi la Polisi tayari limewakamata wahusika kama Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni tarehe 31 Agosti, 2018 ilivyoeleza. Natumia fursa hii kuwakumbusha tena Mgambo wote kuwa makini katika utekelezaji wa maagizo wanayopewa na kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu,” alisema Lugola.

Pia kutokana na tukio hilo, Lugola alisema anazitaka Mamlaka za Majiji, Manispaa na Halmashauri kufikiria kuanzisha Huduma ya Polisi Wasaidizi (Auxiliary Police) katika maeneo yao kwa mujibu wa Sheria ya Polisi na Polisi Wasaidizi Sura ya 322 ili kuepuka matukio ya uvunjifu wa haki za Binadamu kama tukio la Mgambo watatu  jinsi lilivyo tokea.

Aidha, Lugola pia alizungumzia kuhusu baadhi ya matukio mengine ambayo watu  wanajichukulia Sheria mkononi na kuwaadhibu kwa kuwapiga watu wengine kwa sababu mbalimbali.

Aliyataja matukio hayo ni pamoja na ugomvi wa kifamilia ndani ya ndoa ambao huhusisha Wanaume kuwapiga wake zao au wake kuwapiga waume zao, pia  wananchi kuwapiga watu wanaowatuhumu kwa makosa mbalimbali, pamoja na walimu kuwapiga wanafunzi kinyume cha sheria.

Pia Lugola aliwaonya baadhi ya Askari Polisi ambao wanatumia nguvu isiyo ya kadiri kulingana na mazingira halisi wanapowadhibiti watuhumiwa.

“Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Mambo ya Ndani ya Nchi inalaani vikali matukio ya kujichukulia Sheria mkononi na kupitia kwenu Wanahabari nawataka Watanzania kufuata sheria za nchi kwa kuacha vitendo vya kujichukulia Sheria mkononi. Vitendo hivi pamoja na kusababisha uvunjifu wa amani vinaweza kuleta madhara kwa watu ambao hawana makosa na kuichonganisha Serikali na wananchi wake,” alisema Lugola.

Kutokana na matukio hayo, Lugola aliwataka wanandoa wanakumbushwa kutumia Dawati la Jinsia katika Vituo vya Polisi kote nchini ili kuwasilisha malalamiko yao ya unyanyasaji wa kijinsia ndani ya ndoa ili hatua stahiki zichukuliwe.

Pia aliwataka wananchi waendelee kuheshimu sheria za nchi na kuepuka kujichukulia unakuta mtu anapigwa hata haulizi anayepigwa amekosa nini nae anajiunga nao na kumpiga hali ambayo imesababisha majeraha, vilema vya kudumu na vifo kwa watu wasio na hatia.

Hata hivyo, Lugola aliwaonya walimu kwa kufanya matukio kujirudia kwa kuwaadhibu wanafunzi kwa kuwachapa na kuwapiga hovyo kiasi cha kusababisha maumivu makali, ulemavu na vifo.
 
“Natumia fursa hii kuwakumbusha Walimu kote nchini kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo ya Adhabu kwa wanafunzi ambayo imetolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kuepuka madhara yake, kuondoa hofu kwa wazazi na kufanya shule zetu kuwa mahali salama kwa watoto wetu,” alisema Lugola.

Rais Magufuli Kushudia Utiaji Saini Wa Mkataba Wa Ujenzi Wa Meli

Rais Dkt John Magufuli leo Septemba 03, 2018 ameshuhudia  utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa meli mpya na chelezo katika Ziwa Victoria, tukio hili limefanyika Jiji Mwanza na kurushwa moja kwa moja na TBC1, Azam Tv, ikulu.go.tz
Mkataba huo utahusisha ujenzi wa meli moja mpya, chelezo ya kujenga meli hiyo, ukarabati wa meli ya Mv Victoria na Butiama katika Bandari ya Mwanza Kusini jijini hapa.

Meli hiyo mpya itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo pamoja na magari madogo 20 na itafanya safari zake kati ya Mwanza na Bukoba kupitia bandari ya Kemondo, Mwanza na Musoma na pia, Mwanza na bandari za nchi jirani za Kenya na Uganda.

Imeelezwa kuwa mkataba mwingine ni wa ukarabati mkubwa wa meli ya Mv Victoria yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 200 za mizigo, iliyokuwa ikifanya safari zake kati ya Mwanza na Bukoba kabla ya kusitisha mwaka 2014 kutokana na kuharibika kwa mitambo yake. Ukarabati huo unatarajiwa kuchukua miezi 12.

Meli nyingine itakayofanyiwa ukarabati ni MV Butiama yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 100 za mizigo, meli ambayo ilikuwa ikifanya safari zake kati ya Mwanza na Nansio Ukerewe kabla ya kuharibika mwaka 2010.

Kukamilika kwa meli hiyo kutarahisisha usafiri kwa wananchi waishio kwenye visiwa vya Ukerewe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha atembelea Mazoezi ya timu ya Taekwondo Polisi Arusha.


Na Gasto Kwirini wa Polisi Arusha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng’anzi leo ametembelea mazoezi ya Timu  ya Taekwondo ya Polisi Mkoa wa Arusha yanayofanyika kila siku iioni katika Dojo lilipo Kambi ya Polisi New Line Arusha. 

Alipata fursa ya kuona sehemu ya Mazoezi (Gym), Onesho (Show) ya Taekwondo pamoja na changamoto zilizopo katika Timu hiyo. Aidha amewapongeza wachezaji wa timu hiyo walioshiriki katika Michezo ya Majeshi ya Polisi kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati (EAPCCO) yaliyofanyika  Mkoani Dar es Salaam na kupata Medali mbili ya Shaba na Fedha. 

‘‘Leo nimehamasika kuungana na mazoezi haya hasa kwa kuzingatia yanatija katika kazi yetu, Kwa sababu lengo la mchezo huu ni kujenga ukakamavu na kujilinda binafsi. Kuanzia wiki ijayo nitajumuika nanyi, mwisho wa siku na mimi nivae mikanda kama yenu’’. Amesema Kamanda Ng’anzi.

Pamoja na mambo mengine amehaidi kuzifanyia kazi changamoto walizo nazo hasa la vifaa na muda wa Mazoezi kuingiliana na Ratiba za kazi. Alisema atakaa na viongozi  wenzake kuona jinsi ya kutatua changamoto hizo.

Awali akitoa historia fupi ya Timu, Kocha wa Timu hiyo Shija Makoye alisema timu hiyo inahusisha jumla ya wachezaji kumi na tano (15) ambapo wanapata fursa ya kujifunza mbinu mbalimbali za kujijengea ukakamavu na uwezo binafsi wa kujilinda pindi wanapokabiliana na Adui. Pia  alimweleza changamoto mbalimbali ambazo timu hiyo inakumbana nazo.
 

Picha No. 1. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng'anzi akijaribu moja kati ya vifaa vya mazoezi vilivyo katika GYM ya Polisi Arusha. Kushoto kwake ni Kocha wa Timu hiyo Shija Makoye


Tuesday, August 21, 2018

Serikali Kuja na Bima ya Afya ya Kifurushi....Ndugalile Apiga Marufuku Hospitali Kushikilia Maiti

Naibu  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, amesema Serikali ipo katika mkakati wa kuanzisha bima ya afya ya kifurushi kumwezesha mwananchi kujihudumia kadiri ya uwezo wake.

Amesema hiyo ni kwa sababu bima ya afya iliyopo sasa si rafiki kwa wananchi wengi, hali inayofanya baadhi yao, hususan familia duni, kushindwa kujiunga na huduma hizo muhimu za matibabu.

Kauli hiyo aliitoa juzi Dar es Salaam, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Kigamboni, ikiwa siku ya mwisho  ya kuhitimisha ziara yake ya kukagua shughuli za maendeleo jimboni kwake.

Dk. Ngugulile ambaye pa ni Mbunge wa Kigamboni, alisema Serikali ya Awamu ya Tano imetenga bajeti kubwa ya afya kuliko wakati wowote kwa lengo la kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na uhakika wa matibabu mazuri na salama.

“Kama ilivyo mitandao ya simu, na katika bima ya afya tutakuja na vifurushi tofauti tofauti na hapa kila mwananchi atajihudumia kulingana na uwezo wake, lengo letu ni kumfikia kila mmoja,” alisema Dk. Ndugulile.

Akizungumzia vifaa vya kujifungulia kwa wajawazito, alisema Serikali imegharamia vifaa vyote kwa wanaokwenda hospitali kujifungua na vitagawiwa bure vikiwa kwenye mabegi maalumu yenye nembo ya MSD.

Akitoa ufafanuzi wa malalamiko ya wananchi kuhusu kuzuiwa kwa miili ya wanaofariki katika hospitali za Serikali, Dk. Ndugulile alipiga marufuku kwa hospitali zote kuzuia miili ya marehemu ambayo ndugu zao wameshindwa kugharamia gharama za kuitunza.

Aliwataka ndugu wenye matatizo kuwasiliana na uongozi wa hospitali ili miili hiyo kuruhusiwa kwa utaratibu mzuri.

“Jukumu la Wizara ya Afya ni kuhakikisha wananchi wanapata matibabu ya uhakika na pale inapotokea ndugu wameshindwa kulipia gharama za maiti, ni vema wakafuata utaratibu wa kusaidiwa na hili lifanyike kwa kufuata utaratibu,” alisema Dk. Ndugulile.

Bilioni 11 Zatengwa Kuwanufaisha Vijana Wajikwamue Kimaisha

Vijana 30,000 kutoka Mikoa ya Iringa, Mbeya na Mikoa ya Tanzania Visiwani watanufaika na fursa ya mafunzo ya kilimo na ujasiriamali kupitia Program ya Feed the Future inayofadhiliwa na Shirila la Misaada la Marekani (USAID) ambapo watapewa nyenzo na mtaji yenye thamani ya Sh. Bilioni 11.

Hayo yasememwa jana na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi,Vijana na Ajira, Anthony  Mavunde akiwa mkoani Iringa wakati akizindua Baraza la Vijana la Ushauri wa Mradi.

Mavunde alisema katika mradi huo vijana watapewa nyenzo na mitaji ya kuanzia shughuli za uzalishaji mali, ambapo amelitaka Baraza hilo kuhakikisha malengo ya mradi yanafikiwa hasa katika kumkomboa kijana wa kitanzania na changamoto za ukosefu wa ajira na kumsaidia kufikia malengo yake.

Naye Kaimu Balozi wa Marekani nchini Dk.Inmi Patterson alisema Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza ujuzi wa Nguvu kazi ya Vijana wa Tanzania na kuhamasisha ushiriki wao katika sekta ya kilimo ili kuongeza pato la Taifa zaidi kupitia sekta ya Kilimo ambayo imeajiri Watanzania wengi.

Kwa upande wa  Kaimu Mkuu Mkoa wa Iringa, Richard Kasesela ameahidi kutoa ushirikiano wakati wote wa utekelezaji wa mradi huo ambao utawanufaisha Vijana wa Iringa kwa kiasi kikubwa.

Gari la Ikulu ya Rais wa Kenya laibwa na kukamatwa mjini Moshi nchini Tanzania

Jeshi la polisi linawashikilia watu wawili wakazi wa Moshi kwa kukutwa na gari inayosadikiwa kumilikiwa na Ikulu ya Nairobi nchini Kenya ambayo inasadikiwa kuibwa nchini Kenya tarehe 19 Agosti.

Gari aina ya Nissan V8 yenye Namba za Usajili KCP 184 RV. Lakini ilikuwa imebandikwa T954 DEQ ilikamatwa ikiwa njiani ikielekea Kilimanjaro ikitokea nchini Kenya.  Tarehe 19 kulikuwa na taarifa ya gari aina ya V8 kuibiwa Kenya.

Polisikilimanjaro Yanasa Raia Wa Ethiopia 25 Waliongia Nchini Bila Kufuata Sheria


Jeshi la Polisi linawashikilia raia 25 wa Ethiopia miongoni mwao tisa  ni watoto wenye umri chini ya miaka 18  wakiwa katika kichaka eneo la Himo wakisubiri gari kwa ajili ya kuwavusha kuendelea na safari yao ya Afrika Kusini.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro,Kamishna Maidizi wa Polisi,Hamis Issah amesema raia hao wa Ethiopia walikamatwa na askari Polisi wakati wa doria wakiwa na kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la Baraka itema (25) aliyejitambulisha kama fundi ujenzi .

Raia hao 25 wa Ethiopia wanaendelea kuhojiwa na Idara ya Uhamiaji kwa kusaidiana na jshi la Polisi na kwamba mara baada ya taratibu kukamilika watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria kujibu tuhuma zinazowakabili za kuingia nchini bila ya kibali.


Saturday, June 16, 2018

Macho Yote ya Waafrika Leo Nchini Urusi ni Kwa NIGERIA Itayokabiliana na Croatia

Michuano ya Kombe la Dunia inaendelea tena leo Jumamosi kwa viwanja vinne kuwaka moto nchini Urusi.Katika mechi za jana, timu zote kutoka Afrika zilifanya vibaya kwa kupoteza michezo yake ya kwanza kwa bao 1-0.

Misiri iliyojitupa dimbani bila nyota wake Mo Salah ilifungwa mnamo dakika za mwisho na Uruguay huku Morocco nayo ikiambulia maumivu kwa bao moja pekee la kujifunga dhidi ya Irani.

Timu pekee kutoka Afrika leo, Nigeria, inapewa nafasi ya kutufuta machozi waafrika wote endapo itafanikiwa kuibuka na ushindi  dhidi ya Croatia kuanzia saa NNE  usiku.
Kwa upande wa Croatia, hawana majeruhi na wanategemea kutaja mastaa wote wakiwemo Luca modric,Ivan Rakitic,Vedran Corluka na Mario Mandzukic.

Mshambuliaji wa Croatia Nikola Kalinic amesema, Kitu muhimu sasa ni pointi zote tatu.

Kwa Upande wa Nigeria, Mlinzi wa Nigeria, Leon Balogun, anaweza kukosa mechi baada ya kukosa mazoezi yaliyofanyika Alhamis, na Kenneth Omeruo anasubiri mchezaji Wilfred Ndidi ili aweze kuchukua nafasi yake, pamoja na kwamba alikuwa ana majeraha,Odion Ighalo anaweza kuiongoza safu ya ushambuliaji, akishirikiana na Khelechi Ihenacho.

Kocha wa Nigeria Gemot Rohr anasema, "Timu tunayo kwa muda mrefu, tulikuwa nayo pia kwenye mechi za kufuzu, Nina uhakika tutawafanya Wanaigeria wafurahi."

Thursday, June 14, 2018

Serikali yaongeza ushuru wa Chokoleti, Pipi

Ili kuhamasisha uzalishaji wa ndani, Serikali imetangaza kupandisha ushuru wa forodha kwenye peremende, chokoleti, bazoka (chewing corn) na nyanya zilizosindikwa kutoka nje.

Akizungumza bungeni leo Juni 14, wakati akiwasilisha bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19, Dk Mpango amesema ushuru huo umeongezeka kwa asilimia 10 kutoka asilimia 25 iliyokuwa inatozwa mwaka huu wa fedha mpaka asilimia 35 kuanzia Julai Mosi.

“Lengo la hatua hii ni kulinda uzalishaji wa bidhaa hizo katika viwanda vya ndani, ajira,” amesema Dk Mpango.

Waziri Mpango amesema nchi za Afrika Mashariki zina uwezo wa kuzalisha  chokoleti na kutosheleza mahitaji ya soko.

Ajali ya Basi Yaua Wanajeshi 10 wa JKT

Basi lenye namba za usajili T 755 BAB lililokuwa likisafiri kutoka mkoani Tabora kuelekea mkoani Mbeya, limepata ajali leo Alhamisi, Juni 14, 2018 katika eneo la Igodima jijini Mbeya na kusababisha vifo vya askari 10 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) waliokuwa wakitoka mafunzoni na kujeruhi wengine kadhaa.

Taarifa za awali kutoka eneo la tukio zinadai kuwa, basi lililokuwa limewabeba wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania lililokuwa likitokea Tabora kuelekea Mbeya limepinduka katika mteremko wa Igodima, Mbeya.

Chanzo cha ajali hiyo kimesekana kuwa ni mwendokasi uliopelekea  kukatika kwa ‘break’ kutokana na mteremko mkali katika eneo la Igodima na kuangukia korongoni.

Waziri Mpango: Ukusanyaji wa mapato Ulikuwa Trilioni 21 Mwaka 2017/2018

Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango amesema ukusanyaji wa mapato katika vyanzo vyote kwa mwaka 2017/18 yalifikia Sh21.89trilioni sawa na asilimia 69 kwa mwaka.

Ameyasema hayo leo Juni 14, wakati akisoma bajeti kuu  ya serikali kwa mwaka wa fedha, 2018/19.

Amesema kutofikiwa kwa malengo ya ukusanyaji kumetokana na ukwepaji wa kodi, ugumu wa kukusanya kodi kutoka kwa wafanyabiashara wasio rasmi na hawarunzi kumbukumbu, mazingira yasiyo rafiki ya kukusanya kodi, ugumu na gharama kubwa za kulipa kodi.

Ametaja sababu nyingine kuwa ni pamoja na udhaifu wa kutumia mashine za EFD, mpango mdogo na utegemezi wa sekta ya umma kwa sekta binafsi.

Kuhusu mikopo ya ndani, Dk Mpango amesema Serikali ilikopa jumla ya Sh4.9 trilioni sawa na asilimia 80 ya zilizotarajiwa kukopwa na Serikali ilikopa kutoka soko la nje Sh414 bilioni.

"Fedha hizi zimeelekezwa kwenye miradi ya mkakati," alisema Dk Mpango.

Kuhusu deni la Serikali, alisema limekuwa likiongezeka lakini bado ni himilivu.

"Uwiano kwa pato la Taifa ni asilimia 34 ukilinganisha na asilimia 56 ya ukomo," amesema.

Amesema Serikali imeandaa mkakati wa kulipa madeni na kuzuia ulimbikizaji wa madeni kama wakandarasi na wazabuni.

Pikipiki na Magari ya mashindano nazo kuondolewa kodi

Waziri wa Fedha, Philip Mpango amesema serikali inatarajia kufanya mabadiliko kwenye sheria ya forodha la jumuiya ya Afrika Mashariki inayotoa msamaha wa kodi kwa magari yanayotumika kwenye mashindano ya mbio za magari na kujumuisha pikipiki kwenye msamaha huo.

Waziri Mpango ameyasema hayo leo Juni 14 wakati akiwasilisha bajeti kuu kwa mwaka wa fedha, 2018/19, bungeni.

 “Hatua hiyo inatarajiwa kuhamasisha mashindano hayo na kukuza sekta ya utalii nchini,” amesema

Dk Mpango pia amesema serikali imepanga kuondoa tozo kwa vifaa vya zima moto, tozo ya ushauri kuhusu usalama wa afya.

Amesema hatua za upunguzaji wa kodi na tozo, zitaanza kutekelezwa Julai mosi, mwaka huu

Serikali Yafuta VAT kwenye taulo za kike (Pedi)

 Serikali imefuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT),  kwa taulo za kike (pedi) zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.

Msamaha huo umetangazwa leo Alhamisi Juni 14 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alipokuwa akiwasilisha bajeti  kuu ya serikali kwa mwaka 2018/19.    
                                                                                     “Napendekeza kusamehe VAT kwenye taulo za kike kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa bidhaa hizo kwa bei nafuu kulinda afya ya mama na mtoto wa kike hasa walio vijijini na shuleni,” amesema waziri.

Baada ya kutangaza msamaha huo, Bunge lililipuka kwa shangwe na vigelegele ikizingatiwa ni suala lililokuwa na mchango mkubwa wakati wa mijadala ya hoja za wizara mbalimbali zilizwasilishwa kwenye vikao vinavyoendelea.

Chenge aitaka serikali kuangalia upya katazo la kusafirisha madini ghafi

Mwenyekiti wa Bunge Andrew Chenge ameiagiza Serikali kuangalia upya katazo la kusafirisha madini ghafi (cabon) kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine kwa sababu halikuzingatia athari watakazozipata wawekezaji wa mitambo ya uchenjuaji.

Chenge amesema hayo bungeni leo Juni 14 baada ya kuombwa mwongozo na wabunge wawili Stanislaus Mabula(Nyamagana_CCM) na John Heche ( Tarime Vijini-Chadema).

Miongozo hiyo imekuja baada ya taarifa iliyotolewa na Waziri wa Madini Angela Kairuki  kuhusu utekelezaji wa agizo la Spika la kuzuia usafirishaji wa kaboni,  baada ya hivi karibuni kuombwa mwongozo na Heche kuhusu suala hilo.

Katika majibu yake Kairuki amesema katazo hilo linalenga kuzuia utoroshwaji wa madini, ukwepaji wa kodi, ada za ukaguzi na ushuru wa huduma.

Akifafanua hayo, Kairuki amesema siku tisa baada ya katazo hilo hilo Serikali mkoani Geita imetoa vibali vya uchenjuaji 40 tofauti na vibali saba walivyokuwa wakitoa kabla ya katazo hilo.

Hata hivyo baada ya maelezo hayo Heche aliomba mwongozo  na kusema katazo hilo limewaathiri kiuchumi wafanyabiashara wanaomiliki mitambo ya uchenjuaji.

"Wengine mheshimiwa mwenyekiti walikuwa na mikopo katika taasisi za fedha wamesitishiwa ghafla. Watawezaje kujenga mitambo haraka haraka? “Amesema.

Naye Mabula amesema watu wanataabika kutokana na katazo hilo na kushauri kuwa Serikali inaweza kuongeza udhibiti na ikapata mapato yake bila kuweka zuio.

"Mwaka  2014 Serikali iliruhusu gesi kusafirishwa kwasababu  ni raslimali ya Taifa... Hawa watu wanataabika. Tatizo ni uchenjuaji ama usimamizi? Usimamizi unaweza kuimarishwa na Serikali ikapata mapato yake," amesema Mabula

Baada ya miongozo hiyo Chenge amesema miongozo hiyo imetokana na wabunge kutoridhika na majibu ya Serikali.

“Unapopiga marufuku na kuanza ( utekelezaji) leo leo, unapaswa kuzingatia upande wa pili pawe na nafasi. Mwongozo wangu Serikali muangalie tena lengo ni mpate mapato halali lakini tusitoe mkanganyiko."amesema.

Waziri Mpango: Shilingi ilishuka kwa Shilingi 57 mwaka jana

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema licha ya uchumi kuwa imara lakini thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani ilishuka kidogo.

Akizungumza leo Juni 13, wakati akiwasilisha mwenendo wa uchumi kwa mwaka 2017, Dk Mpango amesema thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ilikuwa ya kuridhisha ikibadilishwa kwa Sh2, 228 kwa dola moja.

"Hadi Desemba mwaka 2016 Dola moja ilikuwa inabadilishwa kwa Sh2, 177 na mpaka Desemba 2017 kulikuwa na tofauti ya wastani wa Sh57.79," amesema Mpango.

Mwenendo huo, amesema umetokana na kuboresha kwa usimamizi, utekelezaji wa Sera thabiti za bajeti na fedha na mwenendo mzuri wa urari wa mapato ya fedha za kigeni.